Category: Jamvi la Kiswahili

  • MTIMA WANGU WAUMA

    MTIMA WANGU WAUMA

    (Picha kwa hisani ya Pinterest)

    Na Abdul Shaban

     

    Mwenye hisani ni nani, kwanza ninawauliza,

    Aeleke mtimani, bila hata ya kuwaza,

    Khatari imesheheni, yupo aloniumiza,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Tangazo nilolitoa, makusudio ninayo,

    Sitaki tena madoa, asije kufata nyayo,

    Awe mtuvu kapoa, atulize nilo nayo,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Ilio kubwa sababu, sasa nakwenda kusema,

    Moyo aliusulubu, hakunielewa vyema,

    Amri zake wahabu, hakutekeleza hima,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Mapenzi aliyapata, nami yake nilipata,

    Yani alikula bata, vijana wanavyoita,

    Uzuri wa kumemeta, kwa hayo mi sikujuta,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Alinikata kauli, usiku hata mchana,

    Niliposema tuswali, hapo yeye alinuna,

    Niliudhika kwakweli, japo nampenda sana,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Wala sikumdekeza, onyo nikampatia,

    Hapa nitakufukuza, kama ukiendelea,

    Hakutaka kusikiza, nikawa na mbili njia,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Apendezea uzuri, ila nikajawa khofu,

    Kama kuswali khiyari, vipi niwe mkunjufu,

    Nahitaji yenye kheri, toka kwa mola Raufu,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Nikafanya maamuzi, yalopendeza kwa mola,

    Nikaitoa simanzi, na shetwani mwenye hila,

    Tamko lenye majonzi, nakuacha kisa swala,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Gumzo likaenea, familia na mitaani,

    Naye akajiendea, kurudi kwao nyumbani,

    Sitaki kuteketea, kwa ghadhabu za manani,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Ukweli nishausema, hayo ndiyo yalojiri,

    Nahitaji mke mwema, kwenye dini yu hodari,

    Nimefika qadetama, nawaageni kwaheri,

    Mtima wangu wauma, nataka wa kunipoza.

     

     

     

  • Sherehe ya Eid-ul-Adha 2022

    Sherehe ya Eid-ul-Adha 2022

    (Picha kwa hisani ya Hindustan Times)

    Na Getrude Prosper

    Mwaka huu wa 2022, nchi tofauti tofauti duniani zimesheherekea sikukuu ya Idd kwenye tarehe tofauti. Baadhi ya nchi zimesherehekea siku ya Jumamosi Julai 9 2022 na zingine zimesherehekea siku ya Jumapili Julai 10 2022. Zaidi ya hayo, Waziri wa Usalama wa ndani, Fred Matiang’i ametangaza kuwa Jumatatu, Julai 11 2022 kuwa siku ya mapumziko ya kuadhimisha sikukuu ya Idd-ul-Adha nchini Kenya.

    Idd-ul-Adha ni siku ya kuchinja na huadhimishwa siku ya 10 ya Mwezi wa Dhul-hijjah, mwezi ambao waislamu huenda kuhiji Makka, Saudi Arabia. Sherehe za mwaka huu nchini Kenya zimekua tofauti kidogo kutokana na hali ya uchumi iliyofanya gharama ya maisha kua juu. Baadhi ya wafanyabishara wanadai kua msimu huu wamepata hasara kubwa kwasababu ya kupungua kwa wateja. Kabla ya mabadiliko ya hali ya uchumi, siku za sherehe hua ni siku za wafanyabiashara kuuza zaidi kuliko siku zingine kutokana na misururu ya watu wanokuja sokoni kununua bidhaa mbambali ikiwemo nguo na vyakula.

    Mwaka huu hamna dalili zozote zile za sherehe kwenye baadhi ya maeneo kama awali kutokana na gharama ya maisha kupanda. Vitu vimepanda bei wanunuaji wamepungua.

  • ANGELLA OKUTOYI ASHINDA MASHINDANO YA WIMBLEDON

    ANGELLA OKUTOYI ASHINDA MASHINDANO YA WIMBLEDON

    (Picha kwa hisani ya The Standard)

    Na Gertrude Prosper

     

    Mchezaji wa tenisi, Angella Okutoyi mwenye umri wa miaka kumi na minane aibuka kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kushinda mashindano ya Wimbledon. Katika mashindano hayo ya fainali, Angella alikuwa akishirikiana na Mholanzi Rose Marie Nijkamp katika timu ya wanawake Julai 9, 2022.

    Baada ya kushindwa katika seti ya kwanza ya 3-6 Okutoyi pamoja na mchezaji mwenzake waliamua kujikakamua na kushinda seti ya pili. Wapinzani hao, Kayla Cross na Victoria Mboko walishindwa (11-9) dhidi ya Nijikamp na Okutoyi (3-6, 6-4).

    Angella amevunja rekodi na kuwa Mkenya wa kwanza kufika katika fainali , akishirikiana na mwenzake Rose Marie, baada ya kuwashinda wapinzani wao Nikola Daubenova kutoka Serbia na Circa Bagaric kutoka Kroeshia (6-3 6-4) katika nusu finali.

  • WAZIRI MKUU WA ZAMANI WA JAPAN, SHIZO ABE AFARIKI DUNIA.

    WAZIRI MKUU WA ZAMANI WA JAPAN, SHIZO ABE AFARIKI DUNIA.

    (Picha kwa hisani ya OneIndiaNews)

    Na Gertrude Prosper

     

    Waziri Mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe amefariki dunia baada ya kupigwa risasi akiwa katika kampeni za chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP) kwenye uchaguzi wa wabunge katika mji wa Nara Magharibi mwa nchi hiyo.

    Abe amefariki dunia hospitalini baada ya kulazwa akiwa mahututi kufatiwa kupigwa risasi katika mashambulizi hayo. Katibu Mkuu wa nchi ya Japan, Hirokazu Matsuno pamoja na Waziri Mkuu Fumio Kishida wamesema hali ya Abe ilikuwa mbaya baada ya kupata shambulio la moyo.

    Mshambuliaji huyo ameshakamatwa na maafisa wa usalama na walinzi wa Abe muda mfupi baada ya shambulio hilo.

    Shinzo Abe ni kiongozi wa zamani wa Japan kutumikia nchi hio kwa muda mrefu zaidi kuliko mawaziri wakuu wengine wote nchini humo. Abe alizaliwa Septemba 21 1954 jijini Tokyo na alianza harakati za kisiasa 1993 alipoteuliwa kuwa mwakilishi wa baraza la juu la bunge kisha akateuliwa kuwa katibu mkuu wa baraza la mawaziri Septemba 2005 kabla ya kuja kuchukua nafasi ya urais wa chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP) mwaka 2006. Abe anatoka kwenye familia ya kisiasa ambapo babu yake alikua Waziri wa nchi hio kwanzia mwaka 1957 hadi mwaka 1960 na baba yake alikua katibu mkuu wa baraza la mawaziri la nchi hiyo, cheo ambacho kinaonekana ni cha pili kwa ukubwa zaidi nchi humo. Abe alikua Waziri mkuu wa Japan akiwa na miaka hamsini na miwili mwaka 2006, kiongozi wa kwanza kijana kuchukua nafasi hiyo. Muhula wake wa kwanza madakarakani uliubikwa na majanga kutokana na matatizo yake ya kiafya na kumfanya ajiuzulu. Alirejea tena serekalini na kutumikia wadhifa wa Waziri Mkuu katika nchi ya Japan kutoka mwezi Disemba mwaka 2012 hadi mwezi Septemba mwaka 2020.

    Abe atakumbukwa kwa sera yake ya kiuchumi akijaribu kufufua uchumi wa Japan uliokua umedorora. Atakumbukwa pia kwa kuongeza bajeti ya ulinzi na kubadili sera ya kijeshi ya Japan iliyodumu kwa miaka sabini. Alipambana pia kuboresha mahusiano yake na China.

  • JULAI 7: SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

    JULAI 7: SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

    1. (Picha kwa hisani ya Mwanaspoti)

    Na Abdul Shaban

     

    Siku hii inalenga kukuza matumizi ya Lugha hiyo kama nguzo ya Umoja, Ustawi na Amani

    Kiswahili ni miongoni mwa Lugha zinazotumiwa zaidi Afrika, na kwa Mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) ni kati ya Lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya Milioni 200

  • TETESI ZA SOKA ULAYA

    TETESI ZA SOKA ULAYA

    Na Abdul Shaban

     

    Nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo

    Nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo, 37, ameafiki haja ya Manchester United ya kusaini mkataba na mshambuliaji mpya. (Express)

     

    Mshambuliaji wa Manchester City Mbrazil Gabriel Jesus

    Tottenham wana matumaini ya kuwapiku mahasimu wao wa kaskazini mwa London Arsenal katika mbio za kumsaka mshambuliaji wa Manchester City Mbrazili Gabriel Jesus kwa ofa ya soka ya Championi Ligi . (Mirror)

     

    Raheem Sterling

    Mshambuliaji wa Manchester City na England Raheem Sterling, 27, amekuwa akiwauliza watu kuhusu maisha katika magharibi mwa London huku klabu ya Chelsea ikiwa na nia naye. (Athletic)

     

    Dau la awali la £21.5m kwa ajili ya Sterling limekataliwa. (Fabrizio Romano)

     

    Chelsea wanaweza pia kumuhitaji mlinzi wa Manchester City mwenye umri wa miaka 27- Mholanz Nathan Ake. (Telegraph, subscription required)

     

    Mshambuliaji wa Chelsea na Ubelgiji Romelu Lukaku

    Mshambuliaji wa Chelsea na Ubelgiji Romelu Lukaku, 29, yuko tayari kurejea katika Inter Milan kwa gharama ya mkopo wa £8.5m pamoja na marupurupu aliyokubaliwabaina ya klabu hizo. (Mail)

     

    Manchester United wanaangalia uwezekano wa kufanya dai jipya kwa ajili ya kiungo wa kati wa Barcelona na Uholanzi mwenye umri wa miaka 25 Frenkie de Jong. (Fabrizio Romano)

     

    Kiungo wa kati wa Wolves na Ureno Ruben Neves

    Kiungo wa kati wa Wolves na Ureno Ruben Neves, 25, yuko katika orordha ya Manchester United ya wachezaji inayoweza kusaini mkataba nao iwapo watashindwa kusaini mkataba na De Jong. (Fabrizio Romano, via givemesport)

     

    Newcastle wamepewa ofa ya fursa ya kusaini mkataba na mlinzi Mivory Coast Eric Bailly, 28, kutoka Manchester United. (Mirror)

     

    The Magpies pia wameambiwa kuwa ni lazima walipe £50m kusaini mkataba na winga wa Bayer Leverkusen na Ufaransa Moussa Diaby. (Sun)

     

    Meneja wa Uholanzi na meneja wa zamani wa Manchester United boss Louis van Gaal alihusika kwa sehemu katika kumzuwia mlinzi wa Ajax Mholanzi Jurrien Timber, 21, kuhamia Old Trafford. (Marcel van der Kraan, Sky Sports)

     

    Ajax wametenga euro milioni 40 (£34.3m) wanazotaka kuzitoza Sebastien Haller, huku Borussia Dortmund wakiwa na nia na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27- kutoka Ivory Coast. (90min)

     

    Sunderland, Huddersfield na Bristol City wameweka dau la nyongeza la have £1m kwa ajili ya kiungo wa kati Muingereza mwenye umri wa miaka 21 anayechezea klabu ya AFC Wimbledon Jack Rudoni. (Sun)

  • SAFARI YA UMAUTI

    SAFARI YA UMAUTI

    Na Abdul Shaban

     

    Maradhi yamenisibu, hadi leo naugua,

    Sasa naona aibu, afya imenipotea,

    Naomba kwake Wahabu, kwa rehema za jalia,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Naumwa nakondeana, dawa haziwezi tibu,

    Na kula siwezi tena, ameshasema tabibu,

    Ndugu wanawaza sana, waketi nami karibu,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Nikitizama kushoto, kisha narudi kulia,

    Baba lamtoka jasho, mama naye analia,

    Kauli ni changamoto, kinywani imepotea,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Muda unakaribia, kwa dalili nilo nazo,

    Mauti yanifikia, hilo halina vikwazo,

    Naona amenijia, asohitaji mawazo,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Sakaratil mauti, nilikuwa nasikia,

    Kiu ndo hakikauki, hata maji ya dunia,

    Makosa hayajifuti, madogo nilodhania,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Siwezi tena kutubu, kwa makosa nilofanya,

    Nimekuwa kama bubu, kwa uzito wake kinywa,

    Mauti yaniadhibu, na roho ninapokonywa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Taarifa zatolewa, wengi wanahuzunika,

    *”Kweli tumeondokewa,na mpendwa bila shaka”*

    Kitandani natolewa, uchafu unanitoka,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Ndugu zangu na rafiki, wote wanalialia,

    Na wengine wameketi, eti wananiombea,

    Du’a zao hazifiki, natamani waambia,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Wanatafutwa wajuzi, tayari kuandaliwa,

    Wanikosha kwa simanzi, na marashi kufushiwa,

    Tayari mekwisha kazi, nje sasa natolewa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Simanzi imegubika, baada ya kutolewa,

    Madeni kutangazika, nadai na kudaiwa,

    Swafu witri zimefika, ninaanza kuswaliwa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Mbiombio napelekwa, kaburini kufukiwa,

    Tayari nimeshazikwa, huku watu wahusiwa,

    Mimi nimeshachafukwa, kwa maswali ninopewa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

     

    Tubuni tubuni jama, kaburi lina vituko,

    Hapa mbavu zimebanwa, natamani rudi huko,

    Walau kwa moja jema, muda tena ndo haupo,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Nashauri walimwengu, tupunguzeni machafu,

    Na tuweni wachamungu, tusimuudhi Raufu,

    Pepo pahala pa mungu, hawapelekwi wachafu,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Wanadamu jihadhari, tusije kuangamia,

    Tusifanye ya khatari, mola atuangalia,

    Tuiandae safari, mema tukisubiria,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

  • ENYI VIJANA

    ENYI VIJANA

    (Picha kwa hisani ya Owlcation.com)

    Na Abdul Shaban

     

    Tulisifu na kulitukuza jina lake siku zote

    Kwa maana anatupenda sisi sote

    Uwepo wake umedhihirika kote duniani

    Siku zote nuru za nguvu zake huonekana hata gizani

    Wakati wa furaha na majonzi na dhiki

    Yeye ndiye dereva wa maisha yetu

     

    Enyi vijana, njooni nyote kwake Jalali

    Yeye ndiye mweza wa yote na aliye halali

    Tujiepushe na yale yanayomchukiza

    Tuwe tayari tuitwapo kusikiza

    Yake masharti kuyafuatilia daima

    Ili maisha yetu yaweze kusimama hima

     

    Enyi vijana, tuwe chombo cha kueneza amani

    Ili mioyo ya wazee na kote duniani iwe na furaha isiyo na kifani

    Tujiepushe na yale yanayoeneza chuki

    Bali tulitengeneza chakula cha ujirani wema kama asali kwa nyuki

    Tupige magoti tusali kwa Mola tukiomba dua

    Kuwa kila siku tuweze kuvutia kama ua

     

    Enyi vijana, yakini tukumbuke tulikotoka

    Tubadilishe yetu mienendo ili tupate kuokoka

    Tusiwe na mioyo mizito ilijaa takataka

    Bali tuombe msamaha kwake Mola mkono wake wa kulia tutakaa

    Tuweze kusimama imara katika imani yetu

    Tukijua ya kwamba mola hujibu maombi yetu

    Na yule amwaminiye hawezi kumwacha ateseke kamwe.

  • KITU KIZITO

    KITU KIZITO

    (Picha kwa hisani ya Dreamstime.com)

    {Na Abdul Shaban}

     

    Nakumbuka siku hiyo, niliketi kitandani,

    Alikuja mbiyombiyo, akalala kifuani,

    Akiwa mwenye kiliyo, kama yuko msibani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Kabla kumuuliza, tatizo ni kitu gani,

    Ambacho kinamliza, akatoka furahani,

    Akanambia sikiza, “ewe wangu wa hubani”

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Na mimi sikupuuza, kulifanyia utani,

    Sauti nikapunguza, ya redio pale ndani,

    Akaanza kunijuza, ili kunitoa dhani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Kwa sauti ya kuimba, kama chiriku mbugani,

    Ndipo akaanza amba, kimtiacho shidani,

    Kuwa eti! Ana mimba, ni yangu si ya fulani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Sikusubiri apoe, ama afike mwishoni,

    Ikabidi niyatoe, niliyonayo moyoni,

    Nikaanza na mayoe, yalonijaa pomoni,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    “Nyonda wangu taratibu, sikiza yangu maoni,

    Japo jambo la aibu, mimba isiyo ndoani,

    Kulea ninawajibu, usiwe mwenye sononi”

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Kwangu ikawa aula, sote tukiwa rahani,

    Nikazidi saka hela, viwe havikosekani,

    Vizurizuri vyakula, matunda pale nyumbani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Ikakatika miezi, kwa rehema za Manani,

    Nikiyatoa malezi, mzuri yenye thamani,

    Akabariki Menyezi, kujifungua mwendani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Huku nikiwa na hamu, nikawasili gangoni,

    Mtoto nimfahamu, aliyetoka tumboni,

    Sikuamini dawamu, nilichoona machooni,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Ayi! Nilipata tabu, sijawahi maishaini,

    Nikaiona ajabu, mbaya isiyo mfani,

    Ati! Napewa mwarabu, na mie hatufanani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Tama naachia nibu, kuongeza sitamani,

    Nyonda hana la kujibu, anaomba samahani,

    Kwa haya yalonisibu, siwezi kutamakani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

  • PENYE SAMIA PANA SULUHU

    PENYE SAMIA PANA SULUHU

    (Picha kwa hisani ya SportsArena)

    {Na Abdul Shaban}

     

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameonyesha nia ya kuomba kuandaa AFCON mwaka 2027 kama Tanzania itapata viwanja vingine vitatu vipya zaidi ya vilivyopo.

    Rais Samia aliyasema hayo wakati akipokea Kombe la Dunia 2022;

    “Kwa sasa tuna hiki cha Mkapa, Amaan Zanzibar, hivyo bado viwanja vitatu tuweze kujihakikishia kufanya maombi ya AFCON 2027 iletwe Tanzania,”

    Alisema Samia huku kampuni ya Coca Cola ikiahidi kujenga viwanja vingine vitatu, kimoja Dodoma na viwili Dar-es-salaam.