Category: Jamvi la Kiswahili

  • Prof.Laban Ayiro azungumzia Elimu ya Utatuzi chuoni Daystar

    Na; Righa Sedellar

    Profesa Laban Ayiro – Naibu Chansela.

    Hivi leo katika makala ya Dau La Elimu na Frank Otieno kwenye runinga ya KTN, Naibu Chansela wa chuo kikuu cha Daystar,Profesa  Laban Ayiro pamwe na Mhadhiri wa chuo kikuu cha Moi,Profesa Violet  Naanyu  na Profesa Lukoye Atwoli wa chuo kikuu cha Aga Khan walichangia pakubwa katika mjadala wa Elimu Ya Utatuzi Masuala (Problem based learning) na kusisitiza kuwa, mfumo huu wa elimu una faida nyingi sana katika maisha ya mwanafunzi.

    Elimu ya utatuzi masuala ni mfumo wa elimu unaolenga kutengeneza binadamu  anayeweza  kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii,anayeweza kujimudu maishani na mwenye maadlili yanayoweza kutegemewa nchini na ulimwenguni.

    Profesa  Laban Ayiro alisisitiza kuwa chuo kikuu cha Daystar kimeshachukua mkondo huu wa mafunzo na kusema,”Katika chuo cha Daystar  Walimu huwa wanaenda madarasani ,wanawapa wanafunzi maswali na kuwaaacha wajadiliane na kutatua matatizo mbalimbali kisha kusahihisha matokeo yao kwani  nia yetu ni kutoa wanafunzi walio kamili baada ya kumaliza masomo yao katika chuo kikuu cha Dasystar”.

    Vilevile,wenza wake Profesa Ayiro walisisitiza kuwa,mfumo huu wa elimu unaweza kuwa wa manufaa zaidi japo walimu  pamwe na serikali yetu ya Kenya itatilia mkazo na kuhakikisha kuwa mfumo huu wa elimu umetiliwa maanani na kila mwalimu kutumia mfumo huu kuwaelimisha wanafunzi vyuoni.

    Aidha ,jopo hili la wataalam wa Elimu lilisisitiza kuwa,kuna haja kubwa sana ya walimu kunolewa zaidi na kufunzwa mfumo mpya  wa elimu ili nao pia waweze kuwafunza wanafunzi vyuoni kwani walimu wa sasa walifunzwa mfumo tofauti wa enzi zao. Imekuwa changamoto kubwa sana kwa walimu hawa kuwafunza wanafunzi kutumia huu mfumo mpya wa elimu.Fauka ya hayo,Profesa Violet Naanyu  alisisitiza kuwa elimu huwa ni safari  kwani huwa kuna mwanzo na huwa kuna lengo kuu la mwanafunzi anaposoma na mwalimu anapofunza. Kwa hiyo,Violet alilonga kuwa kuna umuhimu wa walimu kuwa na ushirikiano na wanafunzi ili pamoja waweze kukamilisha ‘safari’ ya  elimu aisee! Kidole kimoja hakivunji chawa .

    Kaditama,wataalam hawa walitoa maoni yao na kusema kuwa ,japo tunataka mfumo huu wa elimu kutufaidi ifaavyo, itabidi viongozi wa vyuo wafunzwe mbinu mpya ya uongozi. Viongozi wawe wanaokubali maendeleo na kuhakikisha kuwa maendeleo tofauti yanatekelezwa katika vyuo wanavyosimamia.

    Wakufunzi nao  wawe tayari kujadiliana na kukosoana na wanafunzi wasiwe na akili ya kufikiri kuwa ni wao pekee wanaojua yote. Wanafunzi pia walihimizwa kuwa na bidii za mchwa na wawe watu wa kutaka kujua mengi, wafanye utafiti na kutumia utafiti huo kutatua matatizo mbalimbali.

    Kwa uhahika,mjadala huu ulikuwa na mafunzo chungu  nzima na ni ombi langu kuwa wewe kama msomaji wangu utaweza kuyatilia maanani yaliyosemwa na wataalam na kuhakikisha kuwa, polepole  na kwa uhakika unakubali mfumo mpya wa elimu kwani mfumo huu una manufaa kadha wa kadha.

  • SIKUKUU YA MOI YAREJESHWA TENA

    SIKUKUU YA MOI YAREJESHWA TENA

    Picha kwa hisani ya: businesstoday.co.ke

    Na Gladys Sheila,
    gladyshila52@gmail.com

    Katibu wa baraza la mawaziri katika wizara ya mambo ya ndani na uratibu wa serikali ya kitaifa Daktari Fred Matiang’i alitoa taarifa siku ya Jumanne na kuidhinisha sikukuu ya Moi kama sikukuu ya kitaifa.

    Hii ni baada ya uamuzi wa mahakama. Mnamo mwaka wa 2010, sikukuu ya Moi iliondolewa katika orodha ya sikukuu za kimataifa wakati katiba mpya ilizinduliwa rasmi. Mwezi wa Novemba mwaka wa 2017, jaji wa mahakama kuu alipinga uamuzi huo kwa kusema kuwa ni jambo ambalo linakiuka sheria. Mojawapo ya sababu ilikuwa kuwa sikukuu ya Moi haikuwa ya kuadhimisha wananchi au ufanisi wa nchi, bali mtu mmoja.

    “Kulingana na sheria kuhusu Sikukuu (Sura ya 110, Sheria za Kenya) na uamuzi wa mahakama katika Kesi ya Kikatiba Nambari 292 ya 2017, ninatangaza kuwa Oktoba 10, 2019, itakuwa sikukuu ya kitaifa,” Waziri Fred Matiang’i akasema.

    Hata hivyo, Wakenya wengi walikuwa na njia anuwai za kusherehekea siku hiyo. Wengine waliendeleza biashara zao kama kawaida, wengine wakisafiri kukutana na jamaa na familia zao na wengine wakapumzika kutoka kazini.

    Liliofanya sikukuu hii iwe ya kipekee ni kuwa wakenya wengi walitumia muda huu kuwatembelea na kuwapa msaada watoto katika nyumba za mayatima, wajane, wazee waliotengwa na familia zao, walemavu na wengineo kama ishara ya upendo.

    Hali kadhalika, wakenya wengine walikuwa na msimamo tofauti kuhusu maadhinisho ya sikukuu hiyo huku wakifananisha kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Moi kama dikteta.

    Picha kwa hisani ya: Nairobinews.nation.co.ke

  • MCHUANO WA KUKATA NA SHOKA

    MCHUANO WA KUKATA NA SHOKA

    Na: Dorothy Waweru
    dorothywaweru161706@daystar.ac.ke

    Picha: Wachezaji wakijikakamua uwanjani

    Sikukuu ya Moi chuoni Daystar ilisherehekewa kwa mbwembwe, vifijo na nderemo kwani katika uga wa “Santiago Barna Betheli” kama unavyojulikana na wacheza kandanda wengi, mchuano mkubwa ulikuwa ukiendelea. Mchuano huo uliandaliwa na wanafunzi wacheza kandanda ikiwemo; Walter Nalwa, Nicholas Atulo Snr, Cedrick na Dadiseh Olwaga ambao walinuia kujiburudisha katika mchezo huo wa miguu.

    Mchuano huo ulijumuisha timu sita zikiwemo: Blueboys, Rawa, Buffoons, Bomboclats, DCF handball na Fimbu. Timu hizi zilimenyana vilivyo ili kushinda zawadi murwa ambayo ilikuwa ni mbuzi mzima. Timu za Buffoons na Rawa ndizo zilifungua uga huo ambao ulikuwa na utelezi kufuatia mvua kubwa iliyokuwa imenyesha usiku wote.

    Timu ya Buffoons ilijikakamua katika dakika za kwanza huku Caleb Msando akiifungia timu hiyo bao la kwanza naye Nicholas Atulo Snr akifunga bao lao la pili. Timu ya Rawa ilijikakamua katika kipindi cha lala salama ambapo John Lemaiyan aliifungia Rawa bao lao la kwanza. Kitengo hicho cha kwanza cha mchezo kilipotamatika, Buffoons walikuwa wamefunga mabao mawili kwa moja.

    Mashabiki wa timu ya Buffoons walijaa uwanjani wakiimba nyimbo za ushindi kwani timu hiyo ingemchinja mbuzi kama zawadi ya ufanisi wao iwapo wangewashinda wenzao kwenye semifinali. Baada ya dakika chache za mapumziko, timu ya DCF handball ilijitosa uwanjani kumenyana na wachezaji wa timu ya Fimbu. Uzoefu mkuu katika mpira wa mikono wa timu ya DCF handball ulionekana kuwapa mkono uwanjani. Hata hivyo baada ya dakika kumi na tano Wallace kutoka timu ya Fimbu alifunga bao la kwanza. Baada ya dakika zingine tano, DCF handball ilisawazisha kupitia mchezaji Ephantus.

    Baada ya nusu wakati wa mchezo huo, timu ya Fimbu ilifunga bao lingine ambalo liliwawezesha kuibuka washindi katika kitengo hicho kwa mabao mawili kwa moja. Timu ya Blueboys vilevile ilichuana na timu ya Rawa huku wakifunga bao lao la kwanza ambalo lilikuwa la pekee katika mchezo huo hivi basi kuibuka washindi dhidi ya Rawa.

    Hata ingawa jua lilikuwa mtikati, wachezaji wa Bomboclat waliingia ugani kumenyana na DCF handball. Yasemekana kuwa wachezaji wa Bomboclat walikuwa wamekesha wakijitayarisha kwa mchuano huo wa kipekee. Katika dakika za kwanza, Bomboclat ilifunga bao lao la kwanza na baadaye kufunga la pili. DCF handball ilijizolea nunge hivi basi Bomboclat kuibuka washindi.

    Isitoshe, kabla ya semi fainali, Bomboclat ilichuana na Fimbu na wakailaza Fimbu bao moja kwa nunge. Timu zilizofuzu kwenye semi fainali ni Fimbu, Buffoons, Bomboclat na Blueboys. Mechi ya kwanza katika semi fainali ilikuwa kati ya Buffoons na Fimbu. Buffoons walilazwa bao moja la kufunga virago baada ya kucheza kwa ukakamavu mwingi sana.

    Nyuso za wachezaji wa timu ya Buffoons zilijaa simanzi kwani mbuzi alikuwa amewakwepa. Lisilobudi hubidi, Buffoons walidondolewa kwenye mchuano wakabaki kuwa mashabiki tu. “Ni uchungu sana mama kubeba mimba tumboni kwa miezi tisa halafu anampoteza mwana wake. Nasikitika sana kuwa tumeshindwa,” Duncan Olile, kipa wa timu ya Buffoons alisema.

    Timu za Bomboclat na Blueboys zilichuana kwenye mchezo wa pili katika semi fainali huku Bomboclat ikiibuka mshindi baada ya kuilaza Blueboys mabao mawili kwa nunge. Washindi wa semi fainali walikuwa Bomboclat na Fimbu. Wakati ukiwa saa kumi na mbili kamili, mchuano kati ya timu hizi mbili ulianza huku Bomboclat ikifunga mabao mawili mida ya dakika za kumi na tano za kwanza. Japo Fimbu iling’ang’ana kiudi na uvumba kujizolea angalau bao moja, jitihada zao hazikuzaa matunda kwani katika kipindi cha pili cha mchezo huo, Bomboclat ilifunga bao lingine. Bomboclat wakafunga mabao matatu kwa nunge.

    Mbwembwe na shamrashamra zilijaa uwanjani wakati ambapo wachezaji wa Bomboclat walipokabidhiwa mbuzi wao. Wachezaji waliachwa ugani wakisherehekea ushindi wao huku mashabiki wakiungana nao kushangilia ushindi wao.

  • KIVUKIO CHA KIFO

    KIVUKIO CHA KIFO

    Na: Dorothy Waweru
    dorothywaweru161706@daystar.ac.ke

    Picha kwa hisani ya: The Star

    Ni afueni kwa wakenya wote na haswa familia yake Bi. Mariam Kighenda kwa kutolewa katika hindi la Victoria.

    Shughuli hii iliyochukua siku kumi na tatu, imezifanya nyoyo nyingi sasa kupata na utulivu. Aila ya Bi. Mariam sasa inauhuru wa kuzipumzisha mili ya wapenda wao ambao wamesumbuka usiku kucha. Japo bado uchungu upo, tunamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho zao pahala pema peponi.

    Hata hivyo, Shirika la Kenya Ferry limekabiliwa na mashtaka chungu nzima kufuatia ajali iliyotokea katika kivuko cha Likoni. Ajali hiyo ilihusisha kutumbukia kwa gari moja kwenye bahari hindi mnamo Septemba ishirini na tisa mida ya saa kumi na mbili. Gari hilo lilikuwa na abiria wawili, Bi. Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu.

    Yasemekana wawili hawa walikuwa wametoka kuzuru shamba katika kaunti ya Kwale na walikuwa wakirejea nyumbani walipopatana na kifo chao.
    Matukio yaliyojiri baadaye yanaashiria utepetevu mkuu wa shirika la Kenya Ferry katika kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha usalama wa wasafiri.

    Baada ya ajali hiyo kutokea siku ya Jumatatu tarehe thelathini Septemba, Kenya Ferry kupitia mtandao wa kijamii wa twitter ilitangaza kuwa watahakikisha kuna meli nne katika kivukio cha Likoni.

    Wakenya kupitia mtandao huo walituma jumbe zilizosheheni kughadhabishwa kwa usemi wa Kenya Ferry kwani la muhimu lilikuwa kuomba msamaha kwa familia ya walioadhirika badala ya kuwaambia wananchi kuwa feri nne zitatutumika kuwasafirisha abiria hapo likoni.

    Ni jambo la kukereketa maini kugundua kwamba shirika la feri halina mikakati bomba inayowahakikishia abiria usalama wao hasa wakati kuna tukio kama hilo linalohatarisha maisha yao.

    Uchunguzi ambao unaendelea kufanywa umebaini kwamba shirika la feri la humu nchini halina wapiga mbizi ambao wanasafiri katika feri mchana na usiku bali wanawategemea wapiga mbizi katika shirika la Kenya Ports Authority na jeshi la baharini humu nchini.

    Uhai wa mama Amanda na mwanawe haungekatizwa ghafla iwapo shirika la Kenya Ferry lingekuwa na wapiga mbizi katika chombo hicho wakati wa mkasa huo. Wapiga mbizi wangelikuwepo wangefanya hima kuwaokoa abiria hawa punde tu gari lao lilipoanza kuzama.

    Msemaji wa serikali Col Rtd, Cyrus Oguna alipokuwa akitoa taarifa aliwaambia wanahabari kuwa gari lilichukua chini ya dakika moja unusu kuzama kwa hivyo kulikuwa na muda tosha wa kuwaokoa wasafiri hawa.

    Sababu za kucheleweshwa kwa kutolewa kwa miili ya walioaga ni kuwa kuna meli zinazopita baharini kupitia bandari ya Mombasa kufanya biashara ambayo inailetea kaunti ya Mombasa fedha nyingi. Tunaelewa kwamba tukikatiza usafiri wa meli baharini uchumi wa Mombasa utaadhirika pakubwa.

    Sababu ya pili ni giza kali ambayo imeshuhudiwa baharini hivyo wapiga mbizi wanatatizika sana. Tatu ni mawimbi makali yanayovuma baharini hivyo shughuli za uokoaji zinagonga mwamba wakati huo hadi mawimbi yatulie. Lakini ile sababu muhimu zaidi ni kuhakikisha kuwa usalama wa wapiga mbizi na wale wote wanaohusika katika shughuli za uokoaji unadumishwa,” haya yalikuwa maoni ya msemaji wa serikali Col Rtd.Cyrus Oguna.

    Shirika la Kenya Ferry limeshuhudia visa kama hivi vya ajali bali ni hatua chache sasa zimechukuliwa kuimarisha utendakazi wao. Wasafiri hawana uhakika wa usalama wao kwani janga kama hili linaweza kutokea bila usaidizi wowote. Ni bayana kuwa uwepo wa kuwa tayari kukabiliana na mikasa ya baharini ni jambo linalofaa kutiliwa mkazo.

    Feri zote zinafaa kuwa na vyombo vya kuhakikisha usalama wa wasafiri na magari pia. Sheria mpya zinafaa kubuniwa ili kuwe na mpangilio katika feri hizi. Hakuna mtu ambaye anafaa kupoteza maisha yake kupitia kisa cha kuhuzunisha kama hiki.

    Picha kwa hisani ya: citizentv.co.ke

  • UONGOZI UPYA KATIKA KLABU YA DAYSTAR COMPASSION AND CARE CENTER

    UONGOZI UPYA KATIKA KLABU YA DAYSTAR COMPASSION AND CARE CENTER

    Na Gladys Sheila
    gladyshila52@gmail.com

    Picha kwa hisani ya: Joseph Gichari

    Josephndungo55@gmail.com

    Klabu ya Daystar Compassion and Care Center (DCCC) almarufu DC3 iliyoko katika chuo kikuu cha Daystar ilisherehekea uongozi upya. DC3, ni klabu ambayo imekuwepo tangu mwaka wa (2013) huku lengo lake kuu likiwa kufahamisha wanadaystar kuhusu maswala ya afya, kuwasaidia kisaikolojia wanafunzi, wahadhiri, wafanyakazi na jamii ya Daystar kwa ujumla. Klabu hii imekuwa chini ya uongozi wa Bi.Susan Botto ambaye ndiye mratibu wake.

    Siku hii ya ndovu kumla mwanawe, iliyoadhimishwa katika chapeli iliwaorodhesha viongozi wake wa mwaka wa 2019-2020 huku waliowatangulia wakiwakabidhi faili za utendakazi wao. Siku hiyo ya aina yake ilianzishwa kwa tenzi za kumsifu na kumuabudu Mungu, hafla iliyoongozwa na kwaya ya Imela katika chuo kikuu cha Daystar. Hali kadhalika, wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi chuoni Daystar walipokea pipi huku ikiwa kiishara kuwa wasiokwenye ndoa wajihifadhi mpaka wakati wa kufunga ndoa.

    Kilele cha hafla hii ni ufahamu dhabiti wa klabu hicho na wanajopo ambao walikuwa Bi. Emmah Nguli na Bwana Allan Ball ambao ni washauri wa maswala ya saikolojia.

    Matayarisho ya siku hii isitoshe hung’oa habta wiki ikianza huku mada kuu ikiwa kuwahamasisha wanadaystar kufahamu afya zao. DC3 hukakisha kuna vitengo mbalimbali ambavyo vyaweza kuwasaidia kutambua hali zao za kiafya ikiwa upimaji wa ongoezeko au upungufu wa sukari mwilini, uchunguzi wa saratani, kuangaliwa meno na upimaji wa ukimwi. Ukabidhishaji wa nyara kutoka kwa naibu wa msimamizi mkuu wa wanafunzi Bi. Irene Kimani.

    Waliotuzwa walikuwa:
    1. David Obong’o- Rais
    2. Gladys Sheila- Naibu wa Rais
    3. Wilbert Kiprop- Katibu
    4. Kevin Korir- Mweka Hazina
    5. Maureen Minus- Mkurungezi wa Halfa
    6. Chris Waweru- Msaidizi wa Vikundi vya Msaada

    Erick Spira, rais anayeshika timu hiyo mpya mkono, aliwapongeza waliomtangulia na kuwahamasisha wanafunzi kuridhika kwa kasoro wanazojua wanazo kwani zina manufaa maishani. Kwa kuwa chanzo cha jambo ni mwisho wa kingine, timu hiyo ilijumuika na kukata keki ya kusherehekea uongozi upya na uliopita katika ofisi zao za DCCC.

    Kweli sote kama wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi twawatakia viongozi hao kila la heri wanapoongoza wanadaystar.

  • KUNA NINI KATIKA BARABARA YA MAGADI?

    KUNA NINI KATIKA BARABARA YA MAGADI?

    C21B84F3-9D5B-4371-BC87-FD7C59550353wangukanuri181152@daystar.ac.ke

    Na: Wangu Kanuri

    Ilikuwa vuta nikuvute katika barabara ya Magadi baina wanafunzi wa chuo kikuu cha Multimedia na polisi. Wanafunzi wa chuo kikuu hicho waliandamana na kufunga barabara hiyo kufuatia ajali iliyomlaza mmoja wao katika hospitali kuu ya Kenyatta huku akiwa katika hali mahututi. Kamanda wa Langata bwana Gregory Mutiso aliwarai wasafiri kutumia njia mbadala wanapowatuliza wanafunzi hao waliokuwa wamekabwa koo. Ajali katika barabara hiyo zinazotamatisha maisha ya wanafunzi katika chuo kikuu hicho si jambo geni ndio maana maandamano hayo yaliyoonyesha kughadhabishwa kwa wanafunzi na madereva.

    Kwa kutaka kuchukulia haki mikononi mwao kwa mwanafunzi huyo aliye katika mwaka wake wa kwanza na ambaye wiki jana aligongwa na yu katika hali mahututi, wanafunzi hao waliokerwa walistahimili vitoa machozi ambavyo maaskari waliwarushia nao wakiwarushia mawe. Mwanafunzi huyo aligongwa na matatu iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi mno hapo karibu na lango la chuo hicho kikuu. Isitoshe wanafunzi hao walilalamikia polisi kwa kuchelewa kushughulika baada ya mwanafunzi huyo kugongwa.

    Uchungu uliokuwa nyoyoni mwa wanafunzi hao ulidhibitisha kuwa walikuwa wamekerwa na ajali zinazofanyika katika barabara hiyo zinazotamatisha nyoyo za wenzao huku wakikumbuka kuwa mwaka wa 2016 walipoteza wanafunzi  wawili katika barabara iyo hiyo. Zaidi ya hayo, walilalamikia kuongezewa kwa nauli kwa matatu ya tume ya Ongataline na kunyanyaswa na waendeshaji wa magari hayo.

    Japo gari hiyo iliyomgonga mwanafunzi hiyo I katika kituo cha polisi, usakaji wa dereva huyo aliyemgonga mwanafunzi huyo bado waendelea. Hali kadhalika wanafunzi watatu walikamatwa katika maandamano hayo.

  • Umaskini tuuangamize au tuupunguze

    Untitled
    PHOTO COURTESY: ARON MTURI

    Ni wangapi wamekuwa wakipoteza wapendwa wao kila mwaka kwa majanga yasiyoeleweka? Tume­kuwa tukijaribu juu chini kutafuta suluhisho, huku tukiambiwa kuwa kuna madaktari ambao hukesha wakitafuta dawa za kati ya magonjwa makuu yanayoangamiza binadamu. Kufikia sasa, bado watu wanatamani kupata suluhisho la jinsi watakavyopata dawa za magonjwa sugu kama vile UKIMWI…lakini la kushangaza ni kuwa hata ugonjwa wa Malaria unaweza kuti­bika, lakini kila siku, takriban watoto ELFU TATU wanaangamia. Ninavyofikiria ni kuwa, tumekuwa watu wanaojishughulisha na mengi hadi tunasahau madogo ambayo tunaweza kuyaondoa kwa haraka.

    Katika Jamii, vijana wana mengi am­bayo wanaweza kuyafanya ili kushughulikia hili tatizo la umaskini, lakini tuseme ukweli, TUMEZEMBEA! Nilifurahishwa sana na jumbe niliyoipata kutoka kwa vijana kadhaa wa chuo kikuu cha Daystar ambayo ilikuwa hivi, “Tumekualika katika mkutano wa vijana, am­bapo tutakuwa tukiongea kuhusu jinsi sisi kama vijana tunaweza kuangamiza umaskini.”

    Singetaka kukuelezeeni jinsi nilivyofika mkutanoni…nilifika mapema, na si uongo, nilitabasamu tangu hadi mwisho. Mkutano wenyewe uliongozwa na Bwana mmoja, Dan Orero, kwa kusema kuwa angependa kila mtu atoe maoni yake. Kivumbi kikaanza! Kwanza, Bwana mmoja aliamka na kusema kuwa kul­ingana na utafiti wa wataalam, imesemekana kuwa si rahisi KUUANGAMIZA umaskini. Tunaloweza kufanya ni KUUPUNGUZA… Kimya! Orero naye hakusema kitu, aliandika tu.

    Zaidi ya hayo, aliuliza kama tunapaswa kui­lalamikia serikali kuhusu kiwango cha juhudi za kuupunguza umaskini. Hili lilimfanya Bwana mmoja kusema kuwa hatupaswi kuitupia seri­kali lawama, kwani haiwezi kufanya kazi bila kushirikiana na wananchi. Kisha, mwengine aliongeza kuwa tunazo rasilimali za kutosha na pia uwezo chungu nzima, ambao tumekuwa tukiupata tangu shule ya msingi, na kuna njia ambazo tunaweza kuzitumia ili kuupunguza umaskini katika jamii.

    Karen, mmoja kati ya wengi waliokuwepo alisema kuwa wazazi wana jukumu kubwa sana katika kuhakikisha kuwa watoto wao watakuwa katika mstari wa mbele katika vita vya kupun­guza umaskini. Ili wazo hili lilete maana, Wa­zazi wana jukumu la kuwaunga mkono watoto wao katika lolote wanalotaka kufanya maisha­ni. Aliongeza kuwa watu wengi wamepata sha­hada, na wamekaa miaka kadhaa bila kazi kwa­sababu walichokifanya chuo kikuu hakiendani kamwe, na kilichokuwepo myoyoni mwao.

    Hakuna aliyenifurahisha kama bwana mmoja, Gordon Odhiambo, aliyeongea kwa lugha ya kiingereza, “let us not come to school to GET JOBS, but to GIVE BACK TO THE COMMUNITY.” Ijapokuwa mimi si gwiji wa lugha ya kiingereza, nilimwelewa na kupasua kicheko. Watu walinishangaa kwa kudhani kuwa alikuwa ameongea upuzi mtupu, bali nilicheka kwani alikuwa ameigonga akili yan­gu kwa maneno ya busara ambayo nilikuwa nimeyatamani kwa muda mrefu.

    Singependa kukueleza mengi, natumai umenielewa, lakini nitakuacha na swali amba­lo wengi wamekuwa wakijiuliza. Je, unafikiri kuwa umaskini unaweza kuangamizwa kabisa, au kupunguzwa tu?

    By: Aron Mturi

    (aronmmtunji@daystar.ac.ke)